Thursday, July 30, 2009

Wapenzi wanavyoaweza kuathirika kwa kutoa Mimba!


Wenyewe wanafanya hivyo wakitoa sababu ya kwamba eti hawajajiandaa kuwa na mtoto kwa kipindi hicho. Swali la kujiuliza ni kwamba, kama hamjajiandaa kuwa na mtoto kwanini hamkuwa makini wakati wa kufanya lile tendo la ndoa?
Kwani kondom hazikuwepo ama mlikuwa hamjui namna ya kutumia kalenda katika kuzuia mimba? Huo ni ulimbukeni na kama itatokea hivyo itaonesha wazi hamko makini katika uhusiano wenu.

Tukiachana na hilo, ni wazi kwamba kila mtu anaifahamu raha ya kuwa na watoto katika maisha hasa kwa wale walio katika ndoa. Kila mtu anapenda kuitwa baba ama mama fulani hali inayowafanya walio wengi kufanya kila linalowezekana ili mwisho wa siku waweze kupata mtoto.

Naamini sote tu watu wazima na tunaelewa wazi kwamba mtoto hawezi kupatikana kimiujiza wala kwa maneno matupu, ni lazima tendo takatifu la ndoa lifanyike tena kikamilifu.

Wataalam wa mambo ya afya wanaeleza kwamba kuna mazingira fulani ambayo yasipokuwepo hata mfanye tendo hilo usiku na mchana ni vigumu kwa mwanamke kupata mimba. Ni vizuri basi wanandoa wakajiweka karibu na watu wa afya ili kufahamu njia sahihi za kuweza kupata mtoto na kwa wakati muafaka.

Lakini sasa, licha ya kwamba raha ya ndoa ni watoto kuna umuhimu mkubwa wa kujiwekea utaratibu mzuri wa kujipatia watoto hao. Si kwasababu raha ya ndoa ni watoto basi mzae tu bila mpango.

Kuna wanaume wengine wanahusudu sana ngono. Kila wakati wanataka kutimiziwa na wake zao na tena hawako makini katika kujizuia na mimba zisizotarajiwa. Matokeo yake ni mimba mfululizo kiasi cha kumfanya mama adhoofike kiafya na pia watoto wakikuwa wakiwa hawana afya nzuri.

Kwanini msijiwekea kiwango kwamba mngependa kuzaa watoto wangapi ambao mtamudu kuwapatia huduma za msingi kutokana na kipato chenu? Kwanini mwanaume asijadili na mwenza wake juu ya watoto wao wapishane kwa umri gani ili wawe makini hata wanapokuwa wanafanya tendo la ndoa? Hayo ni mambo ya msingi yanayoweza kuwafanya muione raha ya kuwa watoto katika maisha badala ya watoto kuwa karaha ndani ya nyumba.

Hakuna kitu ambacho kinawachukiza watu kama wanandoa kufikia hatua ya kutoa mimba eti kwasababu hawakupenda wapate mtoto kwa wakati huo. Kwanini hamkuwa makini tangu awali mpaka mfikia hatua ya kukiua kiumbe ambacho hakina hatia?

Kwa taarifa yako sasa, wengi waliokuwa na tabia ya kutoa mimba kila mara, huja kupata tabu sana katika kupata mtoto pale ambapo watamhitaji na kama watampata ni kwa shida sana.

Labda nitoe tu ushauri wa bure hasa kwa wale ambao ndio kwanza wameingia katika maisha ya ndoa kwamba pamoja na wale walio katika uhusiano, mtoto ana raha zake katika maisha ya binadamu na kama utapata leo kisha ukaitoa mimba jua kwamba unajiweka katika mazingira ya kumkosa mtoto huyo katika maisha yako yote. Upo ushahidi katika hilo.

Kwa maana hiyo wale wenye tabia ya kutoa mimba watambue kwamba kwanza wanajiweka katika hatari ya kupoteza maisha yao, pili wanaweza kutopata watoto tena pale watakapowahitaji na tatu wanapata dhambi kubwa kwa Mungu kwa kitendo hicho cha kinyama. Naamini wapenzi mmenisoma vilivyo. Tuonane tena wiki ijayo .

0 comments: