
Katika makala iliyopita, niliandika mlolongo wa hadithi 12 za ukweli nilizowahi kuambiwa na baadhi ya wanawake waliowahi kuwa na mimba, zilitokea bila kutarajiwa au kupangwa.
Bila shaka unaweza ukaongezea nyingine zinazohusiana na kuwa na mimba bila kutegemea, kwani mwenye mimba ya aina hii huisi inaingilia maisha, shughuli, mategemeo au kazi zake.
Mimba imekuwa kero, imeleta shida, wasiwasi, mzozo, usumbufu na taabu, kwa Kiingereza zinaitwa ‘inconvinience’.
Katika makala hii, tuangalie wanawake wa aina hii, wataamua vipi kuendelea kulea mimba na kuzaa au kutoa mimba.
Katika hali hii wapo ambao hadithi zao nilizoelezea wataiacha mimba ikue na kuzaa mtoto.
Siyo kwamba wao mimba haiwapi shida, usumbufu, wasiwasi, mzozo, kero na taabu, ni kwamba wameamua kwa sababu limetokea.
Wameamua ingawa mimba itabadilisha maisha yao na hata uhusiano. Japo ni kero, shida, wasiwasi, mzozo, usumbufu, taabu lakini watairuhusu hiyo mimba iendelee na watajifungua.
Wanaona kuwa mimba si mwisho wa dunia. watasema “Liwalo na liwe, mimba nitalea, mtoto nitazaa”. Suala la kuitoa mimba haliwaingii kabisa kichwani.
Wana msimamo kama mgombea urais wa Chama cha Republican huko Marekani na ilani ya uchaguzi wa chama hicho inayosema kuwa kutoa mimba ni shambulio la kuua kiumbe hai kisicho na hatia na hakina ulinzi.
Wengine wataamua kuitoa, hawa walioamua kutoa mimba kila mmoja ana sababu zake. Kuna wanaodai wanataka waendelee na masomo, wengine wanawaogopa baba na mama zao, jumuiya itamuonaje, mume wake atamuua pengine bosi atamfukuza kazi ama jamii itajua, maana ni mtu mkubwa nchini, anakwepa aibu na kufikiria jinsi gani waumini watamwona kwa kuwa ni kiongozi wa kanisa ama mchungaji.
Sababu hizi ni nyingi na zinatofautiana lakini zote unaweza ukazijumlisha kwa maneno matatu ya Kizungu, ambayo ni ‘convinience’, expediency’, ease. Ikimaanisha utoaji mimba unaleta utulivu, utakuwa poa, utaleta faraja, utatulia, utamaliza mahangaiko, kero, shida, wasiwasi, mzozo, usumbufu na taabu.
Kama kina mama na kina dada hawa wakiamua kuitoa hiyo mimba, nini sababu ya msingi na maana yake ni nini?
Sababu na kusudi la msingi ni kumaliza taabu, mzozo, shida, kero wanavyosema Wazungu ‘The end justifies the means’ yaani, fanya lolote mradi umetimiza azima yako na lengo lako la kutoa kero, aibu, usumbufu.
Kwa hiyo kila mmoja na mimba yake ameishaamua afanyeje, kuna makundi mawili.
Moja limeamua kuilea mimba na kuzaa, hili tuliite ‘K’ maana yake kuzaa na kundi jingine wameamua kuitoa, hili tuliite ‘A’ maana yake (abortion).
Kundi la kwanza ‘K’ yaani walioamua kuilea na kuzaa linagawanyika na kuwa makundi mawili, la kwanza ni wale tangu mwanzo waliamua kuilea. Hili tuliite ‘K1’. Suala la kuitoa halikuwaingia akilini.
Kundi la pili ‘K2’, limefikiria kuitoa lakini baadaye likaaamua kuilea japo lilikuwa linafikiria kuitoa au kutoitoa.
Tofauti kati ya ‘K1’ na ‘K2’ ni kwamba ‘K1’ hakufikiria kuwa kuna njia mbili, alijua kuwa njia ni moja tu, kuzaa na kulea. ‘K2’ alifikiria kuna njia mbili, kuzaa na kutoa mimba na mwisho kuamua kuilea na kuzaa.
Kwenye kundi (A) ambalo limeamua kuitoa kuna makundi mawili (A1 na A2). A1 ni wale ambao walifikiria kuitoa au kutoitoa na mwisho kuamua kuitoa. A2 ni wale ambao hawakufikiria kuitoa au kutoitoa na walipojua kuwa wana mimba walienda moja kwa moja kuitoa.
Kwao kutoa mimba ni kama kunywa maji pale unaposikia kiu. Anahisi ana mimba, moja kwa moja anaenda kuitoa.
Katika kufikia uamuzi wa kuitoa na kutoitoa bila shaka kila mmoja kwa kujua au kutojua, kwa kusudia au kutokusudia kulikuwa na mambo yaliyokuwa yakimwongoza kichwani mwake.
Kwa kundi la kwanza K1 ambalo pamoja na kero, usumbufu, matatizo na mengineyo, wameamua kuilea mimba bila hata kufikiria, kuitoa ni utu wao, dhamira au labda dini yao.
Kwa jinsi wasivyoweza kufikiria kutoa mimba, wao wanafikiri utoaji mimba ni kuua. Wana msimamo juu ya kuheshimu miili yao, wanajua katika kutoa mimba, mtoaji anagusagusa, anawaingia kwa kutumia vyombo sehemu ya miili yao.
Wazo hilo kwa hali walivyo na utu, kibinadamu wanaona haiwezekani. “Wacha hayo matatizo, kero na usumbufu viendelee lakini siwezi nikaua kiumbe changu tumboni, sitaki mtu aniguse mwili wangu, aniingie mwilini na hasa pahala nyeti,” wanasikika kwa nyakati tofauti wakisema watu hao.
Kuna ambao uamuzi wa kutotoa unatokana na woga wa kudhurika wakati wanapoitoa kwani wameishasikia na hata kuona vifo, taabu, kutozaa na matatizo mengi yatokanayo na utoaji mimba.
“Wacha tu nilee hii mimba nisije kufa nikiitoa, nisije nikawa tasa, nitoke damu nyingi hata kuongezewa damu na ndugu wote wajue kuwa nimetoa mimba, nisije nikachanika vibaya ndani na nje.
“...Nimeishasikia kuwa kunatokea hata kizazi kupasuka unapotoa mimba na kusababisha upasuliwe tumbo lote kutoa kizazi na baada ya hapo huzai tena.
“...Nasikia unaweza ukafa, juzi tu kwenye magazeti msichana wa miaka 16 amepoteza maisha wakati akitoa mimba huko Arusha,” wanasema.
Wanaoamua kuitoa bila hata kufikiri huenda wakawa na matatizo, wengine labda wameishatoa au wameona rafiki zao walitoa na wako salama kama yule mtoto wa kidato cha nne ambaye mdogo wake yupo kidato cha kwanza ana mimba.
Wengine wameishasikia wenzao wakitoa mimba na wako salama na shida ziliisha. Huyu mtoto wa kidato cha kwanza alishasikia kuwa dada yake mkubwa wa kidato cha nne ametoa mimba na sasa anamaliza masomo.
La msingi ni kuwa wanaotoa wanafikiri kufanya hivyo kutamaliza kero, shida, matatizo na tabu.
Uamuzi wa kutoa au kutotoa mimba ni wa mtu binafsi, hata kama kuna mtu labda marafiki au mume mnaomshauri na kumshawishi mtu atoe au ailee uamuzi wa mwisho ni wake.
Katika kufanya uamuzi ni vizuri mtu akawa na habari na hata takwimu fulani zinazomsaidia kuamua kufanya au kutofanya hivyo.