Wednesday, August 19, 2009

Vipi mama uwe bwii na mtoto mgongoni kasinzia?


Pombe au kama inavyoitwa kiheshima na watumiaji wake, kinywaji, ni kimiminika kinachochukuliwa kama kiburudisho na wengi wa watumiaji wake. Kwao ni burudani tosha wakipatapo - iwe ni kwa vijana au wazee - wote ni kuburudika tu.

Kutokana na mapenzi makubwa ya kiburudisho hicho, watu wengine hawawezi kabisa kuipitisha siku hivi hivi bila ya kupata japo kinywaji kiduchu kwa siku.

Nikiwa mmoja kati ya wale wanaoona kinywaji kuwa miongoni mwa burudani kama burudani nyingine, natambua wazi kuwa utakapozidisha kiwango cha kinywaji kichwani mwako, hapo huwa si burudani tena bali ni kero tupu.

Kwa maana pombe ukiiendekeza ni lazima itakuadhiri, kwa hali hiyo kama ‘mwenzangu na mie’ huna uhakika na kiasi gani cha pombe unachoweza kukimudu, kwa kweli ni heri ukae mbali na kinywaji, tafuta starehe nyingine, si kung'ang'ania na kuishia kutia aibu mbele za watu wengine.

Na hapo ndipo stori za ajabu ajabu zinapoanza kutokea, wengine kuanza kupiga kelele, wengine kujisaidia hapo hapo walipoketi pamoja na vituko vingine kibao visivyostahili kufanywa mbele ya kadamnasi na mtu mwenye akili zake timamu.

Katika hali iliyoonyesha kuwa wapenzi wa pombe ni wengi lakini si wote wenye ubavu wa kustahimili kinywaji, wiki iliyopita nilistaajabu sana kumuona mama mmoja akibadilika ghafla kutoka mama mwenye heshima na kuwa mama ambaye mbali ya kukosa adabu, vile vile alikuwa anahatarisha maisha ya mtoto wake mchanga kwa jinsi alivyokuwa chakari!

Mama huyo ambaye kwa mahesabu ya ghafla hakunywa zaidi ya chupa tatu za ‘laga’, lakini alionekana kuwa amelewa vibaya sana huku akiwa kambeba mgongoni mtoto ambaye na yeye alikuwa hoi kwa usingizi mzito!

Kama ningekuwa nimekutana naye huyo mama barabarani, kwa kweli nisingeamini kiurahisi kama ni mtu mwenye akili zake timamu, hisia zangu za awali zingenituma kuwa labda ni mwendawazimu, lakini kwa kuwa alinikuta sehemu ya kinywaji akiwa na akili zake zote timamu kichwani mwake, hapo ndipo nilipoyakumbuka maneno ya hayati Marijani Rajab aliyoyatumia katika moja ya nyimbo zake wakati wa uhai wake, "pombe si chai," kwa maana kasi ya mama huyo kubadilika kimaadili ilikuwa ni kubwa sana tofauti na alivyokuwa mwazoni.

Kadri dakika zilivyokuwa zikisonga mbele ndivyo na yeye heshima yake ikuwa inazidi kuporomoka.

Ingawaje hata mimi ni mmoja wa binadamu wanaotumia kinywaji kama burudani yao, na hasa wakati ule mifuko ikiwa na kitu kidogo. Lakini sikubaliani kabisa na tabia kama ya huyo mama ambaye licha ya kutambua kuwa ana mtoto mdogo mgongoni, yeye aliendelea kuukata mtindi hadi kufikia hatua ya kutotambua kabisa kuwa yuko wapi na yupo na watu gani. Kwa maana kama angetambua kuwa yupo na mtoto wake mchanga, bila shaka asingethubutu kuzidisha kiwango cha kinywaji kiasi cha kumfanya ashindwe hata kuamka hapo alipokuwa ameketi na mtoto wake.

Mbali ya kuwashangaza watu waliokuwa hapo baa kwa kitendo chake cha kwenda viwanjani na mtoto mchanga, ilishangaza zaidi kwa kuonekana kuwa ni mtu anayethamini zaidi kinywaji kuliko hata usalama wa maisha ya mtoto wake na heshima yake mwenyewe mbele ya kadamnasi!

Hata kama una mapenzi sana na kinywaji, kwa nini umtese mototo wako mdogo kwa kuzunguka naye sehemu za ulevi hadi usiku wa manane?

Hayo si mambo hata siku moja, kwa nini starehe ya pombe zako iwe mateso kwa mwanao?

0 comments: