Tuesday, August 18, 2009

Kanuni za kuandaa chakula cha watoto wadogo


Katika nchi zinazoendelea kama vile Tanzania kuna idadi kubwa ya watoto hasa wenye umri chini ya miaka mitano, wanaokufa kutokana na magonjwa ya tumbo. Mfano wa magonjwa ya tumbo ni kipindupindu, homa ya matumbo (Typhoid fever), kuhara damu, n.k.

Moja ya vyanzo vikubwa vya magonjwa hayo ni vyakula wanavyokula watoto kila siku. Ili kulikabili janga la hapo juu, elimu juu ya kanuni za kuandaa vyakula kwa watoto wadogo ni sharti la kwanza. Kwa kukidhi haja hiyo, makala ya wiki hii inachangia kwa kutazama kanuni (principles) kuu saba.
 

Kupika vyakula vizuri

Mara nyingi vyakula vibichi kama vile nyama ya kuku (ng'ombe, mbuzi, n.k.), samaki, maziwa, mboga mboga na kadhalika huwa vijidudu rinavyoweza kuambukiza maradhi.

Hata hivyo, vyakula vikipikwa vizuri vijidudu vingi kama sivyo vyote hufa. Kwa hiyo, ili kutimiza lengo hilo lazima vyakula hasa vya watoto wadogo vipikwe kwa muda wa kutosha ( vizuri).
 

Usiweke chakula kilichopikwa kwa ajili ya mtoto
Pika chakula kitakachomtosha mtoto na umpe mtoto chakula hicho kabla hakijapoa sana. Kwa maneno mengine, mtoto asipewe chakula kilichopoa (kipolo). Kama mtu hana uwezo kiuchumi na anachakula kilichobaki (kipolo) kwa ajili ya mtoto wake, ni lazima chakula hicho akipashe moto kabla ya kumpa mtoto. 

Usichanganye chakula kilichopikwa na kibichi
Kama tulivyoona awali, vyakula vibichi huwa na vijidudu vyenye kusababisha maradhi. Kwa hiyo, chakula kibichi kukichanganya na kile kilichopikwa, matokeo yake ni kuwa chakula kilichopikwa nacho hupata hivyo vijidudu vyenye kuambukiza maradhi.

Vile vile chakula kilichopikwa kisishikwe kwa mikono wala kisiwekwe katika chombo kichafu. 

Pika chakula kwa kutumia maji safi na salama

Maji ya kupikia chakula cha watoto wadogo lazima yawe safi na salama. Yaani tumia maji yaliyochemshwa. Hii ni kwa sababu, maji yasiyochemshwa (au yasiyotiwa dawa ya kutosha) yanaweza kuingiza vijidudu vya maradhi katika chakula ulichokipika.

Kama utapika vyakula vinavyokaa jikoni kwa muda mrefu, kama vile wali hakuna haja ya kutumia maji yaliyochemshwa. 

Osha mikono vizuri
Kabla ya kuandaa chakula cha mtoto, lazima uoshe mikono vizuri. Hii ni kwa sababu, mikono ina vjidudu vyenye kuambukiza maradhi. 

Osha matunda vizuri
Matunda au mboga mboga zinazoliwa bila kupashwa moto, lazima zioshwe kwa kutumia maji yaliyochemshwa (au kutiwa dawa ya kutosha). 

Weka jiko katika hali safi
Jiko chafu ni chanzo kikubwa cha vijidudu vyenye kuambukiza maradhi. Kwa hiyo lazima jiko liwe safi. 

0 comments: