Tuesday, December 15, 2009

Hivi ni kweli wanawake wamezoea kudanganywa?


Nimelazimika kuchambua mada hii kutokana na kupokea baadhi ya maswali kutoka kwa wasomaji wangu wakiuliza juu ya hili, wengine wakiwa na mtazamo hasi na wengine chanya.

Hebu soma meseji hii; “Mambo vipi? Mimi ni binti nina mpenzi wangu, tunapendana sana, tatizo hataki ngono, eti hadi anioe kwani ameniahidi atanioa mwaka 2012, wote ni wanachuo fani za Afya. Kwa sasa hataki kunichezea, kasema hana haraka nami. Je, ni mkweli? Nahitaji ushauri wako. 
Nimeona ni bora niulize. Ni mimi Irene. Please reply.”
Nimenukuu ujumbe huo kama ulivyo, bila kupunguza neno lolote kwa makusudi. Nafikiri hata wewe msomaji wangu kuna kitu umejifunza hapo.

Irene naamini na mimi nitakujibu moja kwa moja kupitia mada hii ambayo kiukweli imezaliwa kutokana na swali lako. Vipengele vifuatavyo vitakuweka huru wewe pamoja na wengine mliokuwa mkitatizwa na swali la aina hiyo.

KUTARAJIA MAMBO MAKUBWA
Dhana ya kwamba wanawake wamezoea kudanganywa inatokana na hulka zao wenyewe za kupenda mambo makubwa pindi wanapokutana na wanaume wanaowatongoza.

Hapa kuna mambo mawili ambayo unapaswa kuyaelewa msomaji wangu mpenzi. Kwanza kuna penzi la dhati na lile lisilo la dhati! Hapa naamaanisha kwamba, ikiwa mwanaume atatangaza mambo makubwa hata kama alikuwa hana mapenzi naye ya dhati atalazimika kuwa naye kutokana na yale mambo makubwa aliyoahidiwa na mwanaume huyo.

Anaweza kuamua kuwa naye ama kwasababu jamaa kasema ana ‘mpunga’ wa kutosha, hivyo mwanamke huyo kuwa na nia ya kutesa naye kisha kuachana, lakini kuna ambao wanakuwa tayari kabisa hata kwa ndoa ili aweze kufaidi maisha mazuri, wakati huo kichwani akiwaza jinsi ya kupata mwanaume mwingine wa nje atakayemtuliza mtima.

Katika hili, wanawake wenyewe ndiyo waliosababisha wanaume wengi kuamua kutoa sifa za uongo walinazo ili waweze kuwanasa wanawake wawapendao. Hata hivyo, lazima ufahamu jambo moja muhimu, wanaume wengi ni wajanja sana, hawezi kujisifia mambo makubwa wakati hana mpango wa ndoa na wewe, maana anajua kwamba kuna siku utagundua na kumuacha.

Hii inamaanisha kwamba, mwanaume huyo atazungumza mambo ya uongo ili uingie ‘line’ lakini akishakutumia tu, humuoni tena. Hawezi kusubiri uone udhaifu wake.

Lakini pia asilimia chache ya wanaume wanaotumia uongo, huwa na nia ya kuoa, lakini kwasababu anafahamu kwamba wanawake wengi hawapendi au hawajazoea kuambiwa ukweli, anaamua kutumia maneno ya ulaghai ili ukubali na mwisho wa siku akishahakikisha amekukoleza vyema kimapenzi, anakuambia ukweli.

“Unajua sweetie lile gari siyo langu, nimemuazima tu mshkaji, lakini sikutaka kukuambia ukweli mwanzoni nikihofia utanikataa, lakini leo naona ni vyema kukuambia ukweli,” hii ni moja ya kauli za kawaida sana kwa wanaume ninaowazungumzia hapa.

Kijana George Macha (33) mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, anaeleza kwamba wanaume walio wengi hawaendi kuzungumza uongo hasa kwa wanawake ambao wameamua kwa dhati kuishi nao baadaye, lakini wanawake wenyewe ndiyo vyanzo vya wanaume kujikuta wakisema uongo kwa lengo la kukubaliwa.

“...nimeoa mwaka wa tano sasa, tayari tuna watoto wawili na mke wangu mpenzi Pamela. Nina uzoefu mkubwa sana katika jambo hili, unajua wanawake hawapendi ukweli, hata Pamela wangu sikumwambia ukweli mwanzoni.

“Nilimdanganya nafanya kazi, naishi kwangu, kwetu uhakika na mambo megine mazuri, lakini baadaye nilipokuja kugundua kwamba mwenzangu ana mapenzi na mimi kama mimi ninavyompenda, ndipo nilipomweleza ukweli kwamba, duka la vipodozi nililokuwa nauza ni la kaka yangu, na pale ninapoishi ni kati ya nyumba za kaka yangu.

“Ulikuwa mzozo mkubwa, lakini baadaye akanielewa. Nashukuru tumeshauriana kimawazo, sasa hivi tuna maduka matatu, tunasaidiana kuyasimamia. Familia ina amani na upendo, lakini nikikumbuka gia niliyomuingilia...nacheka sana...” alisema George Macha, katika mazungumzo nami, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Unayajua maneno ya uongo ambayo wanawake wengi hupenda kuambiwa na wanaume wakati wakitongozwa? Kwanini wanawake wanapenda kudanganywa? Ni sahihi kuendelea kutumia uongo? Ukweli ni upi na utumikeje? 

2 comments:

MARKUS MPANGALA said...

BADO NAFIKIRIA KWANZA NITARUDI PUNDE

Anonymous said...

Kumsubiri mpaka akuoe,je ukikuta hawezi majamboz? au hakufikishi? MamaY.