Thursday, December 17, 2009

Unahisi mpenzi wako anakusaliti? Huu ndiyo mtego kamili


Nakuombea heri kwa Maulana ili afya yako izidi kuwa bora, naamini kwamba ukiwa mzima ndivyo ushabiki wako kwenye Love and Marriage utakavyodumu daima. Wewe ni ndugu yangu.

Macho yako ni kama X-Ray, ukiyatumia vizuri, utamuangalia ndani na nje mpenzi wako na kujua pale wapi anaposema kweli, hali kadhalika utaelewa kule anapokuongopea. Kivipi? Njia ni hizi zifuatazo.

Unapoanza kuhisi kwamba mwenzio hakutendei haki na anacheza ‘game’ la nje, kwanza kabisa anza kuujua ukweli kwa kumdadisi katika maongezi yake. Macho yake yatakupa tafsiri halisi. Huo ndiyo ukweli.

Wanasaikolojia wanasema kuwa binadamu anavyoongea na macho yake ndivyo yanavyothibitisha, maneno yanapotofautiana na macho, kuna walakini katika kile anachokisema.

Pua humuumbua muongo, pindi anapojaribu kudanganya, kwani mara nyingi hucheza kwakuwa anachokiongea hakina hisia zozote. Maneno ya uongo hayatoki moyoni, ndiyo maana hisia hazipo, hivyo viungo havishirikiani.

Anza leo kwa kuongelea habari za watu wanaosaliti mapenzi yao kwa sababu ya tamaa, mtazame usoni jinsi atakavyopokea ujumbe wako. Kuna dalili zozote za uoga amaekuonesha? Kama ndiyo, basi mwenzio si muaminifu.

Mtu safi hana mashaka, anajiamini kwakuwa matendo yake hayana dosari. Muoga maana yake hajiamini, kwahiyo ana nyenendo chafu ambazo hapendi mtu wa kawaida azijue.

Onesha msimamo wako kuwa endapo utabaini kuwa anakusaliti utampiga chini. Mtazame usoni, anakwepa kukutanisha macho na wewe? Jibu, ndiyo, basi huna haja ya kutafuta jawabu lingine. Elewa tu kwamba mwenzako anakuzunguka.

Kitu kingine ambacho ni rahisi kukijua kwa mpenzi wako kuwa anakusaliti ni katika mawasiliano yake, vipi kuhusu simu ya mkononi, hataki uiguse? Kama ndiyo, basi fuatilia.

Mtu anayesaliti penzi lake, huwa mchungu mno kwenye simu ya mkononi kwakuwa ndiko kwenye maovu yake. Anawasiliana na watu wake wa pembeni na hapendi ajulikane.

Muache aende bafuni kuoga, halafu ‘ibipu’, akisikia inaita, atarudi mbio ili apokee. Maana yake unajua ni nini? Jibu, itakuwaje kama aliyempigia ndiye anayekuibia, sasa ukipokea si picha litaungua? Akili kumkichwa!

Mtege leo, mwambie mbadilishane simu zenu, yeye atumie yako na wewe yake. Anakataa? Jibu, ndiyo, basi mwenzako siyo muaminifu. Jiulize, kwanini hajiamini na kuna nini ndani ya simu yake?

Kama nilivyosema awali kuwa mtu msafi hana mashaka kwa sababu nyenendo zake ni nyeupe, aogope nini? Muoga ni mchafu, ndiyo maana hajiamini, anaogoa maovu yake kudhihirika.

Mbali na mawasiliano, mpenzi wako ambaye anakusaliti, siku zote atakuwa ni mwingi wa kukuibulia vikwazo. Hataki kutoka na wewe na mkitoka kuna baadhi ya maeneo hatotaka mkanyage kabisa.

Atakwambia usifike kazini kwake kumpitia wakati wa kurudi nyumbani. Kama mpenzi wako atakupiga marufuku kukanyaga ofisini kwao, unalo swali la kujiuliza. Why? Kwanini?

Jibu la haraka ambalo nakupa ni kwamba anaogopa kugonganisha magari, wewe ukimpitia na mshkaji wake wa pembeni je? Wengine mapenzi kwao ni kufuru, anaweza kuwa nao 10, hapo vipi? Unadhani yupo huru? Ndiyo maana hajiamini!

Pointi ya mwisho, muulize maswali ya kizushi lakini yaliyojaa mitego ndani yake, akijichanganya kujibu, bila shaka jawabu utakuwa nalo kuwa mwenzio anacheza ‘game’ la nje.

Hujawahi kumkamata na mtu mwingine, lakini ghafla unamuuliza hivi: “unadhani ni adhabu gani inayokufaa kwa kunisaliti?” Macho yakimtoka na kuanza kubabaika bila mpango, hali hiyo hiyo itakupa tafsiri ya kuanzia uchunguzi wako.

Swali lingine unaloweza kumuuliza ni hili: “Ni kwa kiwango gani unachukia usaliti kwenye mapenzi?” Jawabu lake, linaweza kukupa kitu cha kuanzia kwenye uchunguzi wako.

Hata hivyo, mbinu hizi zinahitaji busara, baadhi ya watu wana uoga wa asili. Kwa maana hiyo, mtege mwenzio huku ukiangalia matokeo yake. Kuna utofauti mkubwa kati ya uoga wa asili na ule wa kukwepa siri zake kujulikana. Mpaka wakati mwingine...

Alamsiki

2 comments:

MARKUS MPANGALA said...

Mmmmmmmmh!

Anonymous said...

Ni kweli shost kwa hayo uliyotueleza wanawake wenzio. Manake asilimia kubwa ya wanaume hawapendi cm zao ziguswe na wake/girlfriend zao kwasababu watagundua mabaya yao wanayofanya.

Mwanjy