Tuesday, February 16, 2010
Wanawake mliozidi miaka 35,msisahau kuzuia mimba! ZINAINGIAA
Wataalamu wamewapa tahadhari wanawake walio na umri mkubwa kwamba wasijisahau kutumia dawa za kuzuia uzazi, wakiamini kimakosa kwamba hawawezi kupata mimba kwa kuwa wamepita umri wa kubeba mimba. Wataalamu wanasema kuwa, ingawa kiwango cha ubebaji mimba hupungua kadri umri wa mwanamke unapopita miaka 30 lakini haimaanishi kwamba wanawake hao hawawezi kubeba mimba wakiwa katika miaka ya 40 au 50. Imeonekana kuwa watu wengi wakipitisha miaka 35 hujisahau na kudhani kwamba hawawezi kupata mimba tena na hivyo huacha kutumia njia za kuzuia mimba suala ambalo limesababisha kiwango cha utoaji mimba katika nchi za Maghribi kama vile Uingereza kwa wanawake wenye umri wa miaka 40 hadi 44 kiwe sawa na cha wasiachana walio chini ya miaka 16.
Kuna sababu nyingi zinazowapelekea baadhi ya wanawake waamue kutoa mimba, mojawapo ni kuhofia hatari ya kuzaa watoto wenye matatizo (abnormalities) tatizo ambalo hutokea sana kwa wanawake wanaobeba mimba katika umri mkubwa. Lakini wataalamu wanasema kwamba sababu nyingineyo ni wanawake waliobeba mimba bila kujua kwa kuwa walidhani hawatapata mimba kwa kuwa wana umri mkubwa.
Kwa ajili hiyo madakatari wanawashauri wanawake wote waliofikisha miaka 35 na kuendelea wachukue tahadhari kuhusiana na mimba zisizopangwa na waendelee kutumia njia mbalimbali za kuzuia uzazi hadi pale wanapofikia kukoma hedhi au menopause, iwapo hawataki kupata watoto.
Kwa kawaida kitaalamu umri mzuri wa kubeba mimba ni kati ya miaka 20 hadi 35. Kubeba mimba kabla ya miaka 20 huweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto kutokana na sababu mbalimbali za kiafya, kisaikolojia na kiuchumi na kubebea mimba baada ya miaka 35 nako kuna uwezekano mkubwa wa kuhatarisha maisha ya mama na mtoto. Mimba zinazobebwa baada ya miaka 35 hambatana na matatizo mbalimbali kama vile shinikizo la damu, kifafa cha ujauzito, kisukari cha ujauzito na kadhalika huku mtoto anayezaliwa akiwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na matatizo ya kuzaliwa (abnormalities). Wataalamu wanashauri kuwa iwapo utapata mimba baada ya miaka 35 ni vyema ufanyiwe baadhi ya vipimo wakati mimba bado ni ndogo ili kujua iwapo mtoto aliye tumboni ana matatizo au la.
By Shally's Med Corner
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment