Monday, January 18, 2010

Si kila mpenzi anafaa kuwa mkeo/mumeo, wengine ni sumu!


Awali ya yote nikutakie wewe msomaji wangu heri ya Mwaka mpya wa 2010, ni matumaini yangu kwamba umeuona ukiwa mzima bukheri wa afya. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwani wapo waliotamani kuuona wakiwa wazima lakini huwezi amini baadhi walikufa siku moja kabla huku wengine wakiuona wakiwa wamelazwa mahospitalini. Yote kheri!...

Mpenzi msomaji wangu, mwaka 2010 usimpe nafasi mpenzi anayeonekana wazi kutokuwa na penzi la dhati kwako. Ni mwaka wa kufanya maamuzi sahihi kwa kuhakikisha unakuwa na mtu ambaye anakupa matumaini ya kuishi naye milele kwa furaha na amani.

Narudia tena kusema kwamba, usikubali kumfanya binadamu mwenzako akayageuza maisha yako yakawa ni ya kutoa machozi kila siku. Mbaya zaidi unatoa machozi yako kwa mtu ambaye halithamini penzi lako. Yanini kuendelea kumkumbatia mtu aina hiyo? 

Au unadhani mwanaume/mwanamke ni huyo tu uliye naye? Ndugu yangu, huu ni mwaka wa kufanya mapinduzi katika maisha yako ya kimapenzi. Ongeza mapenzi yako kwa mtu anayelithamini penzi lako lakini kwa yule anayelipiga teke penzi lako, mpe tiketi ya kukuacha ili uweze kumpa nafasi mwingine ambaye huenda ndiye aliyepangwa kuwa nawe maishani mwako.
Baada ya kusema hayo nirudi sasa kwenye mada yangu ya leo. Kuna watu wengi ambao walifikia uamuzi wa kuishi kama mke na mume lakini baadaye mambo yakageuka na kwenda tofauti na walivyotarajia.

Nukta ya msingi iliyosahaulika ni kwamba walijikuta wakiingia katika penzi lenye nguvu ya soda ambapo gesi ilipoisha, kila mmoja akaanza kumuona mwenzake si chaguo sahihi.

Tunachotakiwa kujua ni kwamba, sera ya uhusiano wa kimapenzi katika muongozo wowote ule ni kila inapoanza siku mpya mvuto wa kimapenzi kuongezeka. Yaani kadiri siku zinavyosogea, mwenzako azidi kukuona bora kuliko jana na kama itakuwa kinyume chake, hapo hakuna penzi la dhati.

Mapenzi ni mamlaka huru ya hisia, mtu kwa ridhaa yake kuukabidhi moyo wake kwa yule aliyemzimikia. Ni vema ukafanya uchunguzi mapema ili kubaini kama uliyenaye anafaa au laa kuliko kuanza safari itakayokukosesha amani katika siku zijazo. 
Tafsiri ya mapenzi ni moyo kuwa huru kila siku kwa ajili kupenda. Wengi wanakosea kwa sababu wana tabia ya kujenga mazoea badala ya kupenda na kupendwa. Siku hizi wanandoa wengi wanaishi kibubusa bubusa kwa sababu si kwamba wanapendana, bali wamezoeana tu.

Hii ndiyo sababu ya wengi kusalitiana na mwisho wa siku ndoa kugeuka ndoano. Ndio maana nasema, usikubali kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya mazoea, kwani kwa kufanya hivyo utakuja kuteseka katika maisha yako. 
Jaribu kuuuliza maswali moyo wako mara mbilimbili na ukujibu kiufasaha, kisha tathmini penzi la mwenzako kwako, ukiona linatosha basi una kila sababu ya kuanza safari ya kuelekea kwenye kuishi kama mke na mume lakini kama una shaka ni vyema ukaangalia ustaarabu mwingine.

Unadhani kila mpenzi anastahili kuwa mumeo au mkeo? Ukweli ni kwamba, sio kila unayeingia naye katika uhusiano wa kimapenzi anafaa kuwa mwenza wa maisha bali kuna ambao ni sumu, ukijichanganya ukatangaza ndoa baada ya kudatishwa katika mambo flani flani bila kuangalia mambo ya msingi, itafika kipindi utajutia uamuzi wako.

Kama ilivyo kawaida kwamba, safari ya maisha ya ndoa huanzia kwenye urafiki wa kawaida. Tumia kipindi hicho basi kuchunguza kama mnapendana kiukweli. Vipi mnavyoelewana? Kutofautiana ni kawaida lakini je hutokea kwa nadra au ndiyo kila siku? Epuka uhusiano ambao utakulazima kutatua migogoro kila siku kabla ya kulala.
Katika kukusaidia, mambo yafuatayo ukiyazingatia ni muongozo sahihi katika kumpata mke/mume sahihi wa maisha yako.

Mawasiliano yakoje?
Yuko makini katika kuwasiliana na wewe? Ukimtumia meseji ni mwepesi wa kukujibu haraka kama mtu wake muhimu. Unapompigia ni mwepesi wa kupokea? Hatengenezi sababu ya kutowasiliana na wewe, daima anaona njia pekee ya kuwaweka karibu hata kama mpo mbali ni kuwasiliana.

Kama mazingira yako hivyo, basi upendo wa kweli upo na hiyo inatosha kuthibitisha kwamba huyo anakufaa. Ukituma SMS naye akachelewa kujibu ni wazi kwamba haoni umuhimu wako kwake.
Anachokupatia unatosheka?

Ukiwa naye unajisikiaje? Umetosheka? Akiwa mbali na upeo wa macho yako inakuaje, unahisi kukosa kitu muhimu sana katika maisha yako? Vipi na yeye yuko hivyo hivyo? Kama jibu ni ndiyo maana yake ni kwamba, mnaendana kwa sababu inaonekana wazi kwamba bila yeye hakuna wewe.

Anakata kiu yako yote? Na upande wake inakuaje? Unamkuna vilivyo? Ikiwa ni hivyo, basi anatosha kuwa mwenzi wako wa maisha. Katika kutosheka ni hata kwenye mapenzi. Mnapokutana faragha anakusafirisha kule unapotaka, pia naye anaridhika na wewe.

Itaendelea...

0 comments: