Thursday, January 7, 2010

Kwanini kila siku unaishia kuachwa?


Mapenzi ni furaha, lakini siyo wote hubahatika kuwa katika furaha hiyo. Makosa fulani yakifanyika, ama kwa kujua au kwa bahati mbaya basi ndiyo mwanzo wa kupoteza furaha katika mapenzi.

Kwa bahati mbaya sana, baada ya kupoteza furaha, ni vigumu kurudisha kwa haraka, hata kama ulikuwa na mwenzi mwingine kwa muda mrefu lakini baada ya kugundua matatizo yake na kuachana naye, utapata shida sana kupata mwingine.

Lakini pia, hata kama utampata ni vigumu sana kumzoea kwa muda mfupi, kuzoea mazingira na kujihakikishia kuwa ndiye mwenzi wako wa kudumu. 

Siyo ajabu sana wapenzi kuachana, lakini inapotokea wewe unakuwa wa kuachwa kila siku, lazima ujue kwamba kuna tatizo, tena tatizo lenyewe lazima litakuwa upande wako. Ni jambo gumu kidogo kupata hekima ya kugundua jambo hili, lakini waliobahatika kupata wamekuwa wakifanya maamuzi ambayo hayawaumizi mioyo yao. 

Haya mambo yanawezekana rafiki zangu. Kwanza ni kukubali kujifunza, kuangalia wapi ulikosea, ni kipindi gani wenzi unaoachana nao wanapatwa zaidi na hisia za kukuacha n.k. Baada ya hapo ni rahisi kusogea mbele zaidi katika kujua jinsi ya kutatua tatizo ulilonalo. Katika mada hii nazungumza zaidi na dada zangu.

Wapo wanawake wengi sana ambao wanahangaika kwasababu ya kuachwa kila siku. Kila mwanaume anayekuwa naye, baada ya muda mfupi tu, anaachana naye! Hajui tatizo, badala yake anaishia kulia tu. Kulia kwako hakutakusaidia lolote kama hutakaa chini na kujiuliza ni wapi kwenye matatizo, ni sehemu gani huwa unakosea!

Kujua chanzo cha tatizo ni mwanzo mzuri sana wa kuelekea kwenye kupata ufumbuzi. Una miaka ishirini na nne tu, lakini umeshakuwa na wanaume tisa! Hili ni tatizo, tena kubwa ambalo linahitaji dawa ya kuponya na siyo ya kutuliza maumivu.
Sikia kilio cha dada huyu: “Mpaka sasa nimechoka, nahisi kama sitakiwi kuwa na mpenzi, maana kila ninayekuwa naye lazima ananiacha. Neno nakupenda halina thamani kabisa katika maisha yangu ya sasa, yaani nimechanganyikiwa kabisa kaka Shaluwa. Utanisaidiaje niweze kupenda tena?”

Hayo ni maneno ya dada Hilda wa Sinza jijini Dar es Salaam, ambaye alipata kuzungumza nami ofisini kwangu hivi karibuni, jijini Dar es Salaam.

Kilio kama cha Hilda kipo kwa wanawake wengi sana nchini. Hilda aliondoka akiwa mpya baada ya kuzungumza naye kwa takribani saa mbili. Niliongea naye mambo mengi sana, ambayo siwezi kuyaandika yote hapa, lakini kwa uchache sana pitia vipengele vifuatavyo kwa faida yako.

UNAJIRAHISISHA?
Kwanza jaribu kujichunguza kama una tabia ya kujirahisisha. Ni kweli umekuwa na tabia ya kujishusha thamani na kuona kama wewe ni wa kuonewa? Kuchezewa? Mwanaume mwenye ndoto na mwanamke wa baadaye wa maisha yake (mke) hahitaji mwanamke wa aina hii.

Anapenda zaidi awe na mwanamke mwenye msimamo anayetambua thamani yake yeye mwenyewe na maisha yake kwa ujumla. Hapendi mwanamke ‘maharage ya Mbeya’ maji mara moja! Kama utakuwa wa aina hii, hata kama atakuwa amekupenda, ataishia kukutumia na kukuacha, kwani wewe mwenyewe umejionesha kuwa wa aina hiyo.

Mwanaume anapenda sana mwanamke wa kumsumbua kidogo, angalau baadaye apate stori za kusema; ‘lakini mama nanilii ulinisumbua!’. Huu ni ukweli ambao baadhi ya watu wanaukwepa. Acha kujirahisisha!

Kujirahisisha huku ni pamoja na suala zima la kufanya mapenzi, usiwe na haraka na tendo hilo, usiulizie juu ya kufanya mapenzi, lakini kama ikitokea jamaa akataka, usikubali haraka. Onesha msimamo wako, ukiainisha usivyotaka kuchezewa.
CHUNGUZA MIENENDO YAKO...

Wakati mwingine mambo yako yasiyotamanika yanaweza kuwa chanzo cha wewe kuachwa na wenzi wako kila wakati. Angalia tabia zako, tazama mienendo yako, marafiki zako, kauli zako na kila kitu ambacho unadhani kinaweza kuwa tatizo.
Mwanaume hapendi kuwa na mwanamke ambaye ana kampani mbaya, kwani anaamini na wewe pia inawezekana ukawa na tabia chafu kama rafiki zako, lakini kauli nzuri kwa mwenzi pia ni kati ya mambo ambayo mwanaume mwenye nia ya kuoa atavutiwa nayo. Jiangalie upya!

Hii ni mada ambayo ilikuwa na msisimko mkubwa zaidi kwa mwaka huu, ilichangiwa na wasomaji wengi zaidi na nimeirudia leo kama nilivyoahidi wiki iliyopita, lengo likiwa ni kukumbushana sababu za wapenzi wengi kuachwa. Wiki ijayo tutaendelea na mada hii, usikose kwani itabadilisha maisha yako.

2 comments:

Anonymous said...

Hello,mimi ni mdada wa miaka 28 sasa, nina tatizo moja,mimi siishii kuachwa bali naacha kila mwanaume ninayejihusisha naye kimapenzi huwa ninaanza kwa nguvu za soda kisha baada ya mda naanzakumchambua madhaivu yake moja baada ya nyingine kisha naishia kumuacha mataani,sasa sijui nina matatizo au sijakutana na wa kwangu? naomba unisaidie.

Anonymous said...

Hi, Nina mfano wa rafiki yangu ambaye ni binti ila kwasasa ana miaka 33 ila maisha yake yote hajawahi kuwa na mwanaume ni bikra ila cha kushangaza ule msimamo wake wa kutokufanya kila kitendo kinamsababishia mpaka leo hajaolewa kila anayekuawa nae anamuacha almost 4 of them wamemuacha kisa hataki kutoa mamboziiiii. Sasa lipi bora kujirahisi au kutokujirahisi, mm pia kwa mtizamo wangu naweza kuzani ni kuwa tu na true love for both sides.