Tuesday, December 1, 2009

Umemfumania mpenzi wako ‘laivu’, ipi adhabu inayomfaa?

Ni wiki nyingine tunakutana tena kupitia safu hii ambayo kimsingi tunakumbushana na kuelimishana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi. Naamini wewe msomaji wangu umzima bukheri wa afya na uko tayari kabisa kupitishia macho kile ambacho nimekuandalia kwa siku hii ya leo...


Mpenzi msomaji, hakuna kitu kinachouma katika uhusiano wa kimapenzi kama kusikia ama kushuhudia mpenzi wako anakula raha na mtu mwingine, ni kitu kinachouma sana na hiki huwafanya wengine hufikia hatua ya kuchanganyikiwa na hata kuchukua uamuzi wa kukatisha maisha yao.

Kwa wanaume, wengi wanapobaini kuwa wapenzi wao wanawasaliti wamekuwa na kasumba ya kutunisha misuli na kuonesha umwamba kwa kuwatwanga makonde au kuwafanyia vibaya wale waliowanasa nao. Lakini uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa masuala ya mapenzi unaonesha kuwa, ubabe hauwezi kutumika kama njia ya kukomesha tabia ya usaliti.

Kuna wengi ambao waliwafumania wake zao, wakawapiga na kuwajeruhi, lakini wakajikuta hawakukomesha tatizo, zaidi ya kuwapa usugu wapenzi wao wa kuendeleza wizi tena kwa dharau na kejeli huku wakibembelezana kwa maneno kama haya: “Jamaa kasafiri eeh?Njoo basi leo geto tulale usiku mzima “vipi yule bwege alikuuliza jana ulipochelewa kurudi” Huyo jamaa anamuuliza maswali hayo mke au mpenzi wa mtu.

Kama nilivyosema awali, usaliti ni jambo linalouma kwa kiwango kikubwa. Hakuna suala la kuazima mke katika maisha, watu huazimana magari na pesa lakini laazizi, hakuna jasiri wa namna hiyo! Huo ndiyo ukweli wenyewe lakini, kupiga au kuacha unapobaini mpenzi wako amekusaliti kunasaidia? Jibu la kitaalumu ambalo naamini kuna wanaoweza kulikataa ni kwamba hakusaidii. Hakusaidii kwa sababu, ukimpiga hiyo ni adhabu inayoishia hapo hapo, kesho wanakutana, wanakusaliti tena kupozana machungu.

Ukimwacha utakutana nao mitaani wakiwa wameshikana mikono kwa uhuru na raha zao, wewe utaumia sana moyoni mwako. Ukiwaua na wewe utauawa, huku wanadamu wenzako wakikucheka kwa uzembe wa kufikiri. Jamani usaliti upo si tunawaona wake na wapenzi wa watu wanaingizana gesti kila siku?

Hivyo basi, kama hujamfuma mpenzi wako leo kuna siku utakutana na meseji kali za kimahaba zikitoka ama kwenda kwa mwanaume mwingine. Utafanyaje baada ya kubaini hivyo? Maana kama ni tukio basi utakuwa umelishuhudia laivu bila chenga. Wiki hii nataka kutumia safu hii kuwaelimisha wanaume adhabu sahihi ya kumpa mpenzi wako pale utakapomfumania ama utakapobaini anakusaliti kwa namna moja ama nyingine.

Wanaume katika suala hili wanatakiwa kuweka kando mambo ya mabavu. Kwa mfano chukulia mwanaume amemfumania mpenzi wake gesti uso kwa uso akimsaliti na mwanaume mwingine, anachotakiwa kukifanya kwanza ni kupiga moyo konde kisha kuondoka eneo hilo tena kwa kukimbia. Ukifika nyumbani, endelea kunywa maji ili kupoza presha. Akirudi mpenzi wako jitahidi kumkaribisha kwa bashasha, lakini usimuulize ulichoona.

Au kama umenasa meseji za kimahaba kutoka kwa mwizi wako, zitume kwenye simu yako kwanza, kisha baada ya siku ukimaliza uchunguzi wako mtumie tena sms hizo mkeo au mpenzio. Ukifanya hivyo usimuulize, endelea kumpenda na ikiwezekana ongeza matunzo. Nunua ‘mikuku’ akaange kila siku. 

Nakwambia ukifanya hivyo mpenzi wako ataumia sana na hataendelea kukusaliti kwa kuwa atakuwa anawaza unafikiria kumfanya nini? Na kwa yule uliyemshika naye, vivyo hivyo usizozane naye, mwache! 

Utashangaa anahama eneo maana atakuwa anafikiri unamwandalia kombora kumbe wewe wala, umeamua kujituliza tu! Washikaji hii ndiyo dawa ya mtu msaliti. Mwadhibu kwa upole, wanasaikolojia wameithibitisha adhabu hii kuwa ina uchungu ya kupiga au kukemea licha ya kwamba, ni adhabu inayohitaji ujasiri wa hali ya juu.

Kwa leo ni hayo, tuonane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi. 

0 comments: