Thursday, December 10, 2009

'Best Man' anapomtongoza bibi harusi!


Kwa kawaida yule mtu ambaye ni msimamizi wa harusi, yaani Best Man, kama aitwavyo kwa lugha ya wenzetu, mtu huyu ndiye anayetakiwa kuwa karibu sana na maharusi, si tu kwa ajili ya siku ile maalumu ya kufunga ndoa, bali pamoja na siku nyingine zote zilizobakia katika maisha ya hao wanandoa aliowasimamia akiwa kama mshauri wao wa karibu katika masuala ya maisha yao ya ndoa.

Pamoja na kwamba sina uthibitisho wa kisayansi wa jambo hili, lakini kutokana na maelezo ya baadhi ya wazee waliodumu katika maisha ya ndoa kwa miaka kadhaa ambao niliongea nao, kati ya vitu walivyokuwa wakivizingatia zaidi enzi zao kabla ya kuamua kumchagua yupi kati ya jamaa zao ili abebe jukumu la usimamizi wa ndoa yaani best man, ilikuwa ni kuangalia tabia pamoja na mwenendo wake wa kimaadili kwa ujumla.Mtu huyo aliyekuwa anategemewa kuwa ndiye best man, hata baada ya siku ya harusi alikuwa anaendelea kuwa ni mtu wa karibu zaidi katika maisha ya maharusi hao aliowasimamia, tofauti na enzi za hao wazee wetu, hivi sasa kitu hiki kinaonekana kuwa na mtazamo tofauti kidogo kwa baadhi yetu katika maisha yetu ya hivi sasa.

Sana sana sasa hivi wengi wetu tunachokiangalia zaidi ni kama tunashabihiana kwa namna moja au ya karibu kimtazamo wa sura na kimaumbile kuliko kitabia.Pamoja na yote hayo, si kwamba ukaribu huo uwe ni wa kila kitu, la hasha.

Ukaribu unaozungumziwa hapa ni ule ambao unatakiwa uwe na mipaka, si ule wa kungoja jamaa akisafiri, basi best man anaanza kutafuta mbinu za kurithi nyumba na unyumba wa hao aliowasimamia ndoa harusi yao.

Ingawa kwa ujumla mambo huenda yakibadilika siku hadi siku, lakini hili la jamaa yangu mmoja ambaye alikuwa ni best man katika harusi fulani iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana jijini Dar es Salaam, kwa ujumla jambo alilolifanya si jambo jema kunyamaziwa, na kamwe haiwezekani likawa ni kigezo cha mabadiliko ya mtazamo wa ma-best men wa kizazi chetu cha karne hii, bali ni upungufu wa mawazo na mwenendo mzima wa maisha yake ya kistaarabu mbele ya jamii na nafsi yake pia!

Tofauti na ma-best men wanavyotakiwa kuwa karibu kwa maisha yanayofuata misingi, mila na desturi zetu, jamaa huyo yeye aliona kuwa kutokana na nafasi aliyoipata ya kuwa best man siku ya harusi ya rafiki yake, huo ndio ukawa mwanya wake pekee mkubwa kwake wa kumwezesha kuwa karibu zaidi na mke wa jamaa yake huyo kwa masuala mengine ya ziadi kuliko yale anayotakiwa kuwa naye karibu kama best man.

Kwa ujumla kama bibiye huyo angekuwa si makini, basi mtego wa huyo best man wa kujifanya kumtembelea na kumhudumia kwa hili na lile mara kwa mara huyo mke wa rafiki yake inapotokea mume wake kasafiri kikazi, basi hadithi ingekuwa nyingine, kwa maana best man alikuwa anakusudia kufanya u-best hadi ndani ya kumi na nane za jamaa yake kwa kutumia ukaribu huo aliokuwanao wa u-best man!

Ni kitendo cha ajabu sana best man anapopanga mipango ya kumrudi jamaa yake na kusahau kabisa kuwa siku ya harusi aliapa kuwa msimamizi mwaminifu wa wanandoa hao kwa kila hali katika maisha yao.

Si tu kwamba ni kitu cha kushangaza, vile vile ni jambo la kusikitisha sana kwa mhusika pale anapogundua kuwa yule aliyekuwa anamwamini kwa kiasi kikubwa hata pale anapokuwa karibu na familia yake, siku ya siku anapomwona akivinjari ndani ya kumi na nane za maeneo yake ya kujidai huku akiwa na dalili zote za kuleta madhara ya kifataki!

Hata kama ni uchu wa tabia chafu ya kupenda wanawake ovyo ovyo, kwa nini usiwatafute hao wasiokuwa na wenyewe badala yake unakwenda kumtongoza mke wa mtu, tena mtu huyo ni rafiki yako, ambaye anakuheshimu wewe kama msimamizi wa ndoa yake?

Kwa ujumla huo si ustaarabu hata kidogo. Tabia hiyo ni chafu kabisa na isiyotakiwa kamwe katika jamii yetu.

Hivi kama ulikuwa ukijijua kuwa huna uvumilivu mbele za wake za watu wengine kwa nini ukubali jukumu la kuwa msimamizi wa ndoa ya mtu ambaye baadaye utaanza kumtolea mate mkewe?

Hayo si mambo hata kidogo, utamtongozaje mke wa rafiki yako uliyemsimamia harusi yake? Huo lazima uwe ni wendawazimu.

1 comments:

Anonymous said...

mimi naona sio uwendawazimu na huyo mwanamke nae anakuwa amependa wewe umeolewa na mume wako kipenzi leo hii unakuja kutongozwa na rafiki wa mmeo na unajua ni rafiki wa damu kabisa hapom unakuwa unataka nini9 ka sio umalaya mwanaume ye ukilegezea kamba anakula mzigo hajali wewe ni nani so wadada wa be careful sana maana huko ni kudhalilisha mmeo na humpendi ushauri wangu wanawake ambao mmeolewa jufunzeni basi kusema no!!!!!!