Saturday, August 29, 2009

DALILI ZA VVU KWA MTOTO

Mtoto aliyeambukizwa VVU mara nyingi huugua mara kwa mara ikilinganishwa na wengine. Hii huambatana na mtoto kutoongezeka uzito.

Inashauriwa zaidi mama kwenda katika kituo chochote cha afya kinachopima VVU ili kupata huduma hiyo. Mtoto anatakiwa kupima pale anapotimiza umri wa miezi 15 au 18 ingawa kuna kipimo kingine kinachoweza kutumika mapema zaidi kabla ya umri huo.

Inapogundulika mtoto anaishi na virusi vya ukimwi, mzazi na jamii inayomzunguka inapaswa kumwonyesha upendo wa hali ya juu na matunzi stahili kama ilivyo kwa watu wazima, kwani watoto hawa wana nafasi ya kuishi maisha marefu na yenye afya.

Wataalamu wa afya wanashauri kumlisha mlo kamili mtoto mwenye virusi vya ukimwi, kupelekwa klinini kupimwa mara kwa mara hasa chembe chembe za CD4 na kwamba kama ni dhaifu na ipo chini ya asilimia 25, mtoto huyo atahitaji kutumia dawa aina ya ARV ambazo hupunguza makali ya VVU.

Upatikanaji na matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya ukimwi unatoa fursa kwa watoto wenye VVU kukua wakiwa na afya njema, kwenda shule, kuishi maisha marefu na hata kuwa na familia,

Pamoja na kuwepo huduma za namna hii wazazi au walezi wengi wamekuwa hawawapeleki watoto kupata huduma ya dawa za kupunguza makali ya ukimwi kutokana na kutoelewa dalili za ukimwi kwa watoto, kwani nyingi hufanana na magonjwa yanayowapata watoto mara kwa mara.

Wengine wamekuwa na uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa kuwapima watoto VVU na kuelewa hali zao ambapo pia jamii haifahamu mahali dawa za kupunguza makali ya ukimwi kwa watoto zinakopatikana, huku wengine wakidhani hupatikana kwa pesa.

Ili kupunguza matatizo ya ukimwi kwa watoto, ni vyema wajawazito wakapima virusi vya ukimwi na watakaokutwa navyo waingie katika mpango wa huduma ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) ili kumlinga mtoto atakayezaliwa.

Wazazi wanaoishi na virusi vya ukimwi wanapaswa kuwaambia watoto wao juu ya hali zao, kwani kunawezekana kuwa na mazingira rahisi ya kuambukizana.

Watoto wanapaswa kujua ukweli kuhusu VVU na UKIMWI ili waweze kujikinga. Wanapaswa pia kusaidiwa kukabiliana na hofu juu ya ugonjwa huu.

Ni muhimu mzazi au mlezi kumwa mwangalifu anapozungumza na kuangalia umri wa watoto unaozungumza nao kuhusu suala hili.

0 comments: