Tuesday, August 4, 2009

Baada ya Miezi Sita - Nahitaji kufahamu nini?


Ni muhimu kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee mara anapozaliwa hadi anapotimiza umri wa miezi sita. Hii ina maana kwamba mtoto asipewe maziwa mengine yoyote, vyakula au vinywaji ikiwa ni pamoja na maji.

Baada ya miezi 6 maziwa ya mama pekee hayatoshelezi mahitaji ya mtoto. Hivyo mtoto aanze kulishwa taratibu vyakula vya aina mbalimbali ili aweze kukua vizuri.


Maziwa ya mama bado huendelea kuwa sehemu muhimu ya chakula cha mtoto mpaka atimize angalau umri wa miaka miwili.

Wakati wa kumlisha mtoto mwenye umri kati ya miezi 6 na 12, daima mpe maziwa kwanza kabla ya kumpa chakula kingine.

Mtoto ana tumbo dogo hivyo huweza kula chakula kidogo kwa mara moja ni vyema alishwe mara kwa mara.

Kama mama ana virusi vya UKIMWI,inawezekana ikawa bora zaidi kumwachisha mtoto kunyonya maziwa ya mama anapotimiza umri wa miezi 6 na kumpa aina nyingine ya maziwa yanayofaa. Ni muhimu aombe ushauri kwa mtoa huduma wa afya ili apewe maelezo zaidi


KUMBUKA

Kati ya umri wa miezi 6 na miaka 2 mtoto bado huhitaji maziwa ya mama kila siku ili kupata nishati na virutubishi muhimu. Kama mtoto hanyonyeshwi atahitaji kikombe 1 au 2 vya maziwa mengine kila siku mpaka atimize miaka miwili au zaidi. Kama maziwa hayapatikani mpe mtoto milo miwili ya ziada.

Epuka kumpa mtoto vinywaji ambavyo havina virutubishi kwa mfano chai, kahawa, soda na vinywaji vya rangi na sukari (juisi bandia). Mpe mtoto maji ya matunda halisi (juisi) kwa kiasi.

Maziwa freshi ya wanyama na maji anayopewa mtoto lazima yachemshwe. Mpe mtoto maji safi na salama kila siku kukidhi kiu yake.

Daima tumia kikombe kilicho wazi kumlishia mtoto. Usitumie chupa au vikombe vyenye mifuniko yenye vitundu vidogo kwani ni vigumu kuvisafisha.

Kuongezeka uzito ni kiashiria cha afya bora na hali nzuri ya lishe. Endelea kumpeleka mtoto kwenye kliniki ya watoto kila mwezi ili kuchunguza afya, kupata chanjo na kufuatilia ukuaji na maendeleo yake.

Mtoto akiwa mgonjwa apewe milo midogo mara kwa mara pamoja na vinywaji kwa wingi ukijumuisha maziwa ya mama.Mhimize mtoto ale vyakula vya aina mbalimbali hasa vile ambavyo anavipendelea. Mara mtoto apatapo nafuu au kupona ongeza kiasi cha chakula na idadi ya milo.

1 comments:

Anonymous said...

Shosti kweli hapa tutaelimika,maana wengine tumekuwa wazazi hata kabla ya muda wetu loh