Friday, July 31, 2009

Mimba uilee wewe, mtoto umbwagie mama yako! INAHUSUUU?


Wahenga walisema, kulea mimba si kazi bali kazi ni kulea mtoto. Ni dhahiri kabla ya kuutoa msemo huo walizingatia mambo kadha wa kadha yanayoizunguka jamii nzima kulingana na hali halisi ya maisha ya binadamu na jinsi anavyotakiwa kuwajibika mbele ya familia yake husika.

Ingawaje msemo huo ulilenga zaidi katika malezi ya mtoto, lakini haina maana kwamba wahenga hawakutambua kuwa kabla ya mtoto kuzaliwa ni lazima malezi ya mimba yawepo, na vile vile kuwa kulea mimba ni kazi nzito pia, ni dhahiri hilo linaeleweka na halina mjadala.

Kwa kupitia msemo huu, wahenga walikusudia zaidi kuwaasa baadhi ya wanawake ambao mara baada ya kujifungua watoto wao salama salimini, basi habari ya matunzo na malezi kwa watoto wao hugeuka kuwa ni kitendawili kisichoteguliwa. Hawa ni wale wazazi ambao bado wanapenda kujichanganya na mambo ya kujirusha zaidi kana kwamba bado ni wasichana wadogo wasio na majukumu mazito ya kifamilia.

Kwa ujumla kwa wanafamilia wanaojali na kuthamini nini maana ya mtoto ndani ya familia yao, punde mtoto anapozaliwa, huwa ni kama nuru ya upendo na faraja kubwa ndani ya familia yao.

Kinachoshangaza hapa ni pale unapojaribu kuangalia suala hili kwa kulinganisha pande mbili tofauti, wakati upande mmoja utawaona wanafamilia wanashangilia na kumshukuru Mungu siku mtoto anapozaliwa, upande wa pili utawaona baadhi ya akinadada wakitafuta jinsi ya kuwatupa watoto wao punde wanapojifungua!

Hapa kwa kweli nashindwa kupata ulinganifu wa mawazo, hasa wa hawa akinadada, kwa kifupi binafsi inaniuma sana pale ninaposikia mtoto katupwa ama chooni au jalalani wakati familia nyingine zikikesha kusali na kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie wapate mtoto bila mafanikio.

Tukiachana na watu wa aina hii, hoja yangu kubwa ya leo ni kuwazungumzia akinadada au akinamama ambao kwa namna moja au nyingine inaonekana kama vile kwao kulea mamba na kuzaa si tabu hata kidogo, lakini linapokuja suala la malezi, hapo ndipo inapokuwa ni mgogoro mtupu, kwa kuwa miezi michache baada ya kujifungua watoto wao salama salimini, hujifungasha na kuhamishia makazi kwa wazazi wao na baadaye huwatelekeza watoto wao huko huko kwa bibi zao na wao kuanza kukata mitaa tena mijini wakijiandaa kufyatua watoto wengine!

Nasema kufyatua watoto wengine kwa sababu suala la matumizi na malezi kwa watoto wao kwao linakuwa kama vile halipo kabisa, ila wanachokijua wao ni kubeba mimba na kuzaa tu, kazi ya kulea inakuwa ni juu ya wazazi wao.

Inashangaza sana kuona kuwa, kuna watu ambao wakishajifungua tu kila kitu huwa ni juu ya wazazi wao, yaani bibi na babu wa mtoto kana kwamba wao (akinadada) kazi yao ni kubeba mimba na kuzaa tu, suala la malezi si jukumu lao!

Na kibaya zaidi, wengi kati ya akinadada wa aina hii utawakuta wana watoto zaidi ya mmoja na kila mmoja wao ana baba yake tofauti, yaani suala la kujali na kuzingatia nyota ya kijani kwao halipo kabisa!

Hivi hao wazazi wenu ambao waliwazaa nyinyi na kuwalea kwa miaka kibao huko nyuma mnataka waendelee kulea hadi lini? Ni dhahiri enzi hizi kwao si za kulea tena, huu ni wakati wao wa kupumzika na kulelewa na watoto wao, yaani nyinyi mnaowabebesha wazazi wenu mizigo yenu ndiyo mnaotakiwa kuwahudumia wao si wao wawalelee watoto wenu.

Haipendezi hata siku moja, kujirusha ujirushe wewe, mimba ubebe wewe, kuzaa uzae wewe, vipi kazi ya kulea mtoto wako umbwagie mama yako mzazi?

Acheni hizo, mnapobeba mimba mnatakiwa mjue pia kuwa kuna kazi ya kulea mtoto mbele yenu, si kufyatua tu na kuwabwagia wazazi wenu kazi ya kulea.

0 comments: