Wednesday, January 20, 2010
Mume anaweza kumbaka mke wake?
Kwa utandawazi ulivyo, wana ‘haki za wanawake’ wanasema NDIYO! Kwanini ndiyo? Kwa sababu kitendo cha kujamiiana kinatakiwa kuwa na ridhaa ya moyo kwa kila mmoja na si suala la mmoja kukurupuka na kutaka ili kukidhi haja yake ya matamanio kwa wakati huo...
Wana ‘haki’ hao wanasema kuwa, mume anaweza kumbaka mkewe kama atakuwa anataka tendo la ndoa, lakini mke huyo hayuko tayari (kwa sababu yoyote ile).
Mfano, mzee James wa Ngarenaro, Arusha alipowahi kuongea na mwandishi wa kitabu hiki kuhusu suala hilo alidai kuwa, mkewe aliwahi kumtamkia kuwa, kumwingilia kimwili bila ridhaa yake ni kumbaka hata kama ni wanandoa. Lakini je, mzee James mwenyewe anasemaje kuhusu kauli ya mkewe?
“Si kweli, nilimuoa kwa maana hiyo, kwamba nitakapokuwa na hamu ya kufanya mapenzi, yeye atakuwepo, sasa kwanini kuwe na ridhaa kwa pande zote, kinachotakiwa mke kuwa na ridhaa wakati wowote kama mume anavyotakiwa kuwa.
Na hata yeye atakapokuwa na hamu ya kufanya mapenzi, mimi nipo.”
Mama Hilda, mkazi wa Kijenge, huko huko Arusha na ni mwana ‘haki’ za wanawake, yeye anapingana kwa kusema kuwa, mume kutaka tendo la ndoa kwa mkewe, wakati mke hayuko tayari si ‘haki’ na ni ubakaji kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na (eti) kinaweza kumfikisha mume mahakamani. “Utamuingiliaje kimwili mwenzako huku unajua hayuko tayari, si haki. Kisheria anaweza kukushitaki na ukahukumiwa,” anasema mama huyo bila haya usoni.
Akaongeza kuwa, maumbile ya mwanamke yalivyo akiingiliwa bila ridhaa anaweza kuchubuka na kupata maumivu makali sana achilia mbali maambukizi ya magonjwa kama yapo.
“Sisi wanawake sehemu zetu za siri ziko delicate sana (nadhani ana maana ya laini). Kwa hiyo kama hatuko tayari kwa tendo la ndoa, huwa ni rahisi sana kupata michubuko na maumivu makali.”
Hata hivyo, kinga ya mama Hilda inakuja kuangushwa vibaya sana na mama Mfaume, wa soko la Kilombero, Arusha huko huko.
Mama Mfaume, anasema yeye ni mwalimu mzuri kwenye sherehe za kufundisha maisha wake watarajiwa (Kitchen Party). Anasema kuwa, moja ya mafundisho ya Kitchen Party siku hizi ni kumwambia bibi harusi mtarajiwa kuwa, ili ndoa yake idumu na kumwepushia mumewe na ‘nyumba ndogo’ ni ‘kumpa’ mumewe haki yake kila anapohitaji.
“Tena huwa tunawaambia kuwa, hata kama unakuna nazi au unafua. Mumeo akirudi nyumbani na kukwambia anataka, mpe. Usimnyime kwani kumnyima kila anapotaka ndiko kunakosababisha kuzaliwa kwa ‘nyumba ndogo’”, anasema mama Mfaume.
Hata hivyo, bado wana ‘haki’ hao wanakuja kupingwa vikali na baadhi ya maandiko ya kiimani. Katika Biblia kuna maandiko yanayosema kuwa, mke au mume hakuna mwenye uwezo juu ya mwili wake ila mwenzake. Kwamba, mkishakuwa wanandoa, mke hana amri juu ya mwili wake wala mume.
Tena kuna sehemu maandiko hayo yanasema ‘msinyimane, mpeane, kama kuachana kwa muda sahihi lakini baadaye mkarudiane tena ili shetani asije akawajaribu.’
Sehemu nyingine maandiko yanasema kwamba, ili kuzuia zinaa ndiyo maana Mungu alimtaka kila mwanaume kuwa na mke wake mwenyewe na si kila mwanamke kuwa na mume wake mwenyewe. Hii maana yake nini? Kwamba, kwa kitendo cha mwanaume kuwa na mkewe, ‘akitaka anapata!’ Kinyume cha hapo ni kwenda kinyume na mipango ya Mungu.
Ila kuna sababu, ambayo mume hatakiwi ‘kumjua’ mkewe kila anapotaka. Mfano, katika hali ya ugonjwa, au kuwa kwenye siku zake (period)!
Hata hivyo, hapa sasa nasema mimi, ieleweke kuwa, dhana hii si kwa mke tu, hata mume. Kwamba mkewe anahitaji na yeye hana kipingamiza, hatakiwi kumnyima ingawa maumbile ya mwanaume kama hayuko tayari hayatoi nafasi kwa mwanamke kuweza kukamilisha kiu yake mwenyewe tofauti na maumbile ya mwanamke.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment